Page 45 - Historia_Maadili
P. 45
Aidha, uhamaji wa wanaume kwenda kufanya kazi mbali ulisababisha kuenea kwa
tabia mpya za mahusiano kati ya wanaume hao na wanawake wa mijini au mashambani
walikokuwa wakifanya kazi. Hali hii ilisababisha baadhi ya wanaume kupoteza
uaminifu na hivyo kusababisha kuenea kwa maradhi ya zinaa na kuvunjika kwa ndoa.
Vilevile, ukoloni ulipandikiza maadili mapya ambayo mara nyingi yalikinzana
FOR ONLINE READING ONLY
na kanuni za asili za jamii. Kwa mfano, uchumi wa kikoloni ulikuza ubinafsi na
ushindani, ambapo watu walihimizwa kutafuta faida za kibinafsi kupitia kazi za ujira,
uzalishaji wa mazao ya biashara na biashara kwa ujumla. Mabadiliko haya yalijenga
ubinafsi ambao ulidhoofisha uhusiano na ushirikiano wa kindugu na kijamii uliokuwa
ukiunganisha jamii za Kitanzania. Pia, wakoloni walileta maadili mapya kuhusu
familia, ndoa na uhusiano wa kijamii. Kwa mfano, ndoa za Kikristo na Kiislamu
zilianza kuchukua nafasi ya ndoa za kitamaduni na hivyo kubadilisha maadili ya
kijamii yanayohusu familia na majukumu ya kijinsia.
Athari za kiuchumi
Kuja kwa wakoloni kuliathiri taratibu mbalimbali za uzalishaji mali katika jamii.
Kabla ya ukoloni, shughuli za kiuchumi kama vile kilimo, biashara, uvuvi na ufugaji
zilifanyika kwa mujibu wa mila na desturi za Kitanzania na kulingana na mahitaji ya
jamii iliyohusika. Shughuli hizi zilifanywa kwa pamoja chini ya mamlaka za jadi.
Hata hivyo, kuingia kwa wakoloni kulibadilisha mfumo mzima wa uzalishaji na
umiliki wa mali. Watu walianza kunyang’anywa mali zao kama vile ardhi, ambayo
ilichukuliwa na walowezi wa kikoloni pamoja na serikali yao.
Zaidi ya hayo, uchumi wa kikoloni uliweka msisitizo kwenye uzalishaji wa mazao
ya biashara kama vile pamba, kahawa, chai na karafuu, ili kuzalisha malighafi kwa
ajili ya viwanda huko Ulaya magharibi. Wakoloni pia walileta uchumi unaoendeshwa
kwa fedha, umiliki binafsi wa mali, pamoja na teknolojia mpya iliyotumika katika
uzalishaji mali. Mabadiliko haya yalisababisha kuibuka kwa matabaka katika jamii,
kuongezeka kwa umaskini, migogoro na hatimaye kumomonyoka kwa maadili.
Umoja na mshikamano uliokuwepo kabla ya ukoloni ulitoweka. Hivyo, mfumo mpya
ulioletwa na wakoloni ulijenga jamii tegemezi na yenye mashindano badala ya umoja
na ushirikiano kama ilivyokuwa hapo awali. Kwa mantiki hii, jamii za Kitanzania
zilianza kutoka kwenye misingi yao ya maisha na kuingia kwenye misingi mipya
ambayo ilitingisha na kuathiri mifumo ya asili ya maadili.
Maadili ya Kitanzania yaliyodumishwa wakati wa ukoloni
Maadili ya jamii za Kitanzania yaliendelea kudumishwa hata wakati wa ukoloni.
37
03/10/2024 18:15:11
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 37 03/10/2024 18:15:11
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 37

