Page 50 - Historia_Maadili
P. 50
Sura ya Tatu Mapambano ya awali dhidi
ya uvamizi wa kikoloni
FOR ONLINE READING ONLY
Utangulizi
Jamii za Kitanzania zilitumia mbinu na njia mbalimbali kuukataa na kuupinga
uvamizi wa kikoloni. Katika sura hii, utajifunza kuhusu dhana ya uvamizi wa
kikoloni na sababu za kupinga uvamizi wa kikoloni. Pia, utajifunza mbinu na
njia zilizotumika katika kuupinga uvamizi wa kikoloni. Umahiri utakaoujenga
utakusaidia kuenzi, kuthamini na kuendeleza harakati za ukombozi dhidi ya
unyonyaji na ukandamizaji wa aina mbalimbali katika jamii.
Fikiri
Mapambano ya jamii za Kitanzania dhidi ya uvamizi wa kikoloni.
Dhana ya uvamizi wa kikoloni
Uvamizi wa kikoloni ni kitendo cha nchi moja kuingia katika nchi nyingine kwa lengo
la kuanzisha utawala wake kisiasa, kiuchumi na kijamii. Mara nyingi, uvamizi huu
hutekelezwa kwa kutumia nguvu za kijeshi. Uanzishwaji wa utawala wa kikoloni
hutegemea kushindwa kwa nchi inayovamiwa kujilinda au kuzuia uvamizi huo.
Uvamizi wa kikoloni nchini Tanzania (Tanganyika na Zanzibar) ulipingwa vikali
kwa sababu jamii za Kitanzania zilifahamu kwamba kuruhusu wakoloni kuvamia
kungesababisha kupoteza uhuru wao.
Kwa sababu za kizalendo na kupenda jamii zao, viongozi wengi wa jamii za Kitanzania
waliongoza mapambano dhidi ya uvamizi huo tangu miaka ya 1880 na mapambano
hayo yaliendelea hata baada ya ukoloni kuanzishwa nchini Tanganyika. Wananchi
walipinga na kuonesha wazi hisia zao za kutokubali dhuluma na unyanyasaji kutoka
kwa wakoloni, hali iliyojitokeza karibu katika kila sehemu ya Tanzania. Mapambano
ya awali dhidi ya wakoloni yalihusisha jamii moja moja, jambo ambalo linamaanisha
kuwa, hatua za mwanzo za kuupinga uvamizi wa kikoloni hazikuhusisha nguvu za
pamoja za jamii mbalimbali za Kitanzania au taifa moja la Tanzania.
42
03/10/2024 18:15:11
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 42
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 42 03/10/2024 18:15:11

