Page 54 - Historia_Maadili
P. 54

Ili kulinda uhuru na maadili ya jamii ya Wanyamwezi, Mtemi Isike aliwaongoza kwa
          ushupavu askari wake kupambana na majeshi ya Wajerumani. Zaidi ya askari 1000
          wa jeshi la Wajerumani walipambana vikali na askari wa Isike. Hata hivyo, ngome ya
          Mtemi Isike ilivunjwa na majeshi ya kivamizi ya Wajerumani. Isike alipoelemewa,
          aliona ni bora ajiue kuliko kukamatwa na Wajerumani, hivyo alijilipua kwa baruti
          pamoja na familia yake mnamo mwaka 1893. Hii inaonesha kuwa Mtemi Isike
        FOR ONLINE READING ONLY
          alikuwa mzalendo wa kweli aliyekuwa tayari kufa kwa ajili ya nchi yake na hakuwa
          tayari kunyanyaswa na wavamizi wa kikoloni.
          Mapambano ya jamii za watu wa pwani: Mapambano ya awali dhidi ya uvamizi wa
          Kijerumani katika ukanda wa pwani ya Afrika Mashariki ya Kijerumani (sasa
          Tanzania) yaliongozwa na wafanyabiashara mashuhuri Abushiri bin Salim al-Harthi
          wa Pangani na Bwana Heri bin Juma wa Uzigua. Viongozi hawa waliongoza
          mapambano dhidi ya sera za unyonyaji za Wajerumani, ambazo zilivuruga na kutishia
          masilahi ya biashara katika ukanda wa pwani na pia kupora uhuru wao.
          Mwaka 1889, Abushiri bin Salim aliwaongoza wananchi wa pwani katika maeneo
          ya Pangani kupigana na  Wajerumani na
          kufanikiwa kuwaondoa katika baadhi ya
          maeneo ya pwani. Kutokana na upinzani
          mkali alioutoa kwa majeshi ya Kijerumani,
          Wajerumani waliomba msaada kutoka kwa
          majeshi ya Uingereza. Muungano huu
          ulisababisha Abushiri kukimbia kwa sababu
          za kiusalama. Kwa kutumia njia ya kugawa
          umoja miongoni mwa jamii za Kitanzania,
          Wajerumani walifanikiwa kumkamata
          Abushiri bin Salim al-Harthi baada ya
          kusalitiwa na Chifu Magaya wa Usagara.
          Mwaka 1889, Abushiri bin Salim al-Harthi
          aliuawa kikatili kwa kunyongwa hadharani
          na Wajerumani huko Bagamoyo. Kielelezo         Kielelezo 3.1: Abushiri bin Salim
          3.1 kinaonesha Abushiri bin Salim.

          Bwana Heri bin Juma aliwaongoza Wazigua wa maeneo ya Saadani dhidi ya uvamizi
          wa Wajerumani. Ingawa baadaye alishindwa, aliendesha mapambano makali ambayo
          yalionesha jinsi wananchi walivyokuwa hawako tayari kunyanyaswa na kunyonywa
          na Wajerumani. Wakati huo huo, mapambano dhidi ya Wajerumani katika maeneo
          ya Kilwa Kivinje yaliongozwa na Hassan bin Omari Makunganya mwaka 1894.
          Kama ilivyokuwa kwa mashujaa wengine, Makunganya alipambana vikali sana
          katika maeneo yake. Hata hivyo, baadaye alikamatwa na kunyongwa na Wajerumani
          huko Kivinje kwenye mwembe ambao mpaka sasa unajulikana kama “Mwembe
          Kunyonga.”


                                                  46




                                                                                        03/10/2024   18:15:12
   HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd   46                                         03/10/2024   18:15:12
   HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd   46
   49   50   51   52   53   54   55   56   57   58   59