Page 52 - Historia_Maadili
P. 52
Sababu za kuupinga uvamizi wa kikoloni na maadili yake
Utawala wa kikoloni nchini Tanzania ulisababisha kupotea kwa uhuru, kudunishwa
na kuharibiwa kwa maadili ya jamii. Wakoloni walidhihaki mila na desturi ambazo
zilikuwa msingi wa maadili ya jamii. Hali hii iliwachochea wananchi, chini ya uongozi
wa viongozi wao hodari na shupavu wa jadi, kuupinga utawala wa kigeni ili kulinda
uhuru, utamaduni na maadili yao.
FOR ONLINE READING ONLY
Aidha, wananchi walinyonywa kwa kulazimishwa kufanya kazi za vibarua na kulipwa
ujira mdogo katika mashamba ya mkonge, pamba, chai, tumbaku na pareto. Wakulima,
wakiwa chini ya usimamizi mkali wa majumbe na wanyapara, walidhalilishwa kwa
kuchapwa viboko. Pia, wananchi walilazimishwa kulima mazao ya biashara kama
pamba, kahawa na chai kwa faida ya wakoloni na mabepari wa Ulaya Magharibi,
ambapo mazao hayo yaliuzwa kwa bei ndogo.
Zaidi ya hayo, mfumo mpya wa kodi ulioanzishwa na wakoloni uliwalazimisha
wananchi kulipa kodi ya kichwa na kodi nyingine kwa pesa tasilimu. Jambo hili
liliwakera sana kwa kuwa hawakuwa na pesa, hivyo walilazimika kuuza mifugo yao,
kufanya kazi za vibarua kwa wakoloni na walowezi au kulima mazao ya biashara ili
kupata pesa za kulipa kodi.
Wakoloni walitumia adhabu za kikatili kama kuwanyonga viongozi wa jamii
za Kitanzania waliopinga utawala na maadili yao. Wananchi pia waliteswa na
kudhalilishwa hadharani kwa kuchapwa viboko waliposhindwa kulipa kodi au
walipotenda makosa mengine dhidi ya utawala wa kikoloni, jambo lililoshusha
heshima, ushujaa na utu wao ambao ulikuwa umejengwa kwa muda mrefu na jamii
zao za asili.
Aidha, ardhi yenye rutuba iliporwa na wakoloni kwa ajili ya kilimo cha mazao ya
biashara, hali iliyowafanya wananchi washindwe kukidhi mahitaji yao ya chakula
kutokana na kuwa na mashamba madogo yasiyo na rutuba ya kutosha. Hatimaye,
wananchi walinyang’anywa udhibiti wa maeneo yao ya biashara kwa mfano, Wahehe
walipambana na Wajerumani walipojaribu kuimarisha na kupanua mipaka yao ya
biashara, jambo lililosababisha chuki na mapambano.
Kazi ya kufanya 3.3
Fanya utafiti mdogo, kisha andika taarifa kuhusu jinsi uvamizi wa kikoloni
ulivyosababisha mmomonyoko wa maadili katika jamii za Kitanzania.
44
03/10/2024 18:15:12
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 44 03/10/2024 18:15:12
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 44

