Page 46 - Historia_Maadili
P. 46
Ingawa kulikuwa na jitihada kadhaa za kubadilisha maadili hayo kutokana na
ushawishi wa wakoloni, bado maadili yaliendelea kuwa nguzo muhimu katika jamii.
Katika awamu ya mwisho ya ukoloni, mawazo ya utaifa na harakati za uhuru yaliibuka
na kuungwa mkono na baadhi ya wazungu wenye msimamo huria. Hali hii ilichangia
kuunda maadili mapya ya kisiasa na kijamii, ambapo watu walihimizwa kujivunia
utambulisho wao wa Kitanzania na kupinga utawala wa kikoloni. Hata hivyo, wakati
FOR ONLINE READING ONLY
wa ukoloni, baadhi ya maadili ya kiutamaduni ya Kitanzania yaliendelea kuhifadhiwa
na jamii za wenyeji. Baadhi ya maadili haya yanaelezwa katika sehemu zinazofuata.
Umoja na ushirikiano: Dhana ya maisha ya jumuiya na uwajibikaji wa pamoja
ilikuwa tunu kuu katika jamii nyingi za Kitanzania. Kwa mfano, miongoni mwa
Wachaga wa Kilimanjaro, kilimo cha jumuiya na kazi za pamoja zilikuwa na umuhimu
mkubwa. Vitendo hivi vilichangia kudumisha mshikamano wa kijamii na kuhakikisha
kwamba hakuna mwanajamii aliyeachwa nyuma, hata katika mazingira ya shinikizo
la utawala wa kikoloni. Shughuli za pamoja kama vile kilimo, ujenzi, au shughuli
nyingine za kijamii zilifanywa kwa manufaa ya jamii nzima ili kuimarisha uhusiano
wa kijamii.
Heshima kwa wazee: Licha ya utawala wa kikoloni, jamii za Kitanzania ziliendelea
kuzingatia kanuni za kiutamaduni zilizosisitiza heshima kwa wazee. Kwa mfano,
jamii za Wazaramo wa eneo la pwani ziliendelea kushikilia maadili haya wakati wa
ukoloni, ambapo wazee walitumika kutoa ushauri na kufanya uamuzi. Aidha, wazee
walikuwa walinzi wa maarifa, mila, ujuzi na mapokeo ya kijamii.
Vilevile, jamii ya Wamasai iliendelea kushikilia tamaduni zao za kuonesha heshima
kwa wazee na viongozi wa jadi. Heshima hii kwa viongozi ilikuwa muhimu kwani
ilidumisha umoja na mshikamano wa kijamii. Hivyo, kudumisha utulivu wa kijamii na
mwendelezo wa utamaduni na maadili, licha ya usumbufu uliosababishwa na ukoloni.
Kwa ujumla, kuheshimu wazee na watu waliowazidi umri kulikuwa na nafasi kubwa
katika jamii nyingi za Kitanzania hata katika kipindi cha ukoloni.
Mifumo ya haki ya jadi: Jamii nyingi za Kitanzania ziliendelea kutumia mifumo
yao ya haki ya jadi katika kutatua migogoro. Kwa mfano, miongoni mwa jamii za
Wasukuma katika Kanda ya Ziwa, kulikuwa na mabaraza ya kimila yaliyowajibika
kusuluhisha migogoro ndani ya jamii. Mabaraza haya, yalishirikiana na mfumo
wa kisheria wa kikoloni lakini yalisalia kuwa chombo muhimu cha kudumisha
sheria na utulivu ndani ya jamii. Jambo hili linadhihirisha uimara wa mifumo ya
utawala wa kimila. Mifano hii inaonesha jinsi tunu za Kitanzania zilivyohifadhiwa
na kubadilishwa wakati wa ukoloni na hivyo kuonesha uthabiti wa mila na desturi
katika kukabiliana na athari za nje.
38
03/10/2024 18:15:11
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 38 03/10/2024 18:15:11
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 38

