Page 61 - Historia_Maadili
P. 61
Matumizi ya silaha duni dhidi ya silaha bora za Wajerumani
Katika sehemu kubwa ya Tanzania, wananchi walioshiriki katika mapambano
hawakufanikiwa kuuangusha utawala wa kikoloni kwa sababu Wajerumani walitumia
silaha bora zaidi kuliko zile zilizotumiwa na wananchi. Kwa mfano, Wajerumani
walitumia mizinga na bunduki, wakati wananchi walitumia pinde, mishale, ngao,
mawe, marungu na majambia.
FOR ONLINE READING ONLY
Usaliti
Baadhi ya viongozi wa jadi waligeuka kuwa vibaraka wa serikali ya kikoloni. Katika
maeneo mengi, baadhi ya jamii za Kitanzania ziliungana na Wajerumani kupigana
na jamii zingine za Kitanzania. Hii ilisababisha jamii nyingi kushindwa vita, kwani
jamii jirani zilizoungana na Wajerumani ziliwasaidia kufichua udhaifu na nguvu za
jamii hizo na hivyo kurahisisha ushindi kwa Wajerumani. Kwa mfano, Wasangu na
Wabena waliungana na Wajerumani kutoa siri na kupigana na Wahehe. Vivyo hivyo,
katika jamii za Wachaga, Mangi Mandara/Rindi aliungana na Wajerumani kumshinda
Mangi Sina.
Maandalizi duni
Wananchi hawakuwa na maandalizi mazuri ya vita ikilinganishwa na wavamizi wa
kikoloni. Wavamizi walikuwa na muda mzuri wa kujiandaa kwa vita, wakati jamii
nyingi za Kitanzania zilijikuta katika vita ghafla, mara baada ya kuona wavamizi
tayari wamevamia. Jamii za Kitanzania zilikuwa hazijamjua vyema adui yao, hali
iliyochangia kushindwa kwao. Maandalizi mazuri ya Wajerumani yaliwafanya
washinde vita kwa urahisi.
Teknolojia duni ya mawasiliano
Wajerumani walikuwa na teknolojia nzuri ya mawasiliano na usafiri, ambayo ilirahisisha
mawasiliano kati ya maeneo mbalimbali. Kwa mfano, waliweza kutumia telegramu
kutuma taarifa za vita kuhusu vifaa na wanajeshi kwa haraka. Hii ilikuwa ngumu kwa
jamii za Kitanzania, ambazo zilitegemea njia za jadi za mawasiliano zilizochukua
muda mrefu kufikisha ujumbe kwa walengwa. Pia, Wajerumani walitumia magari na
vyombo vingine vya usafiri vilivyowarahisishia harakati zao, huku wapiganaji wa
Kitanzania wakitumia muda mrefu kutembea kwa miguu.
Uchumi dhaifu
Jamii nyingi za Kitanzania zilikuwa na uchumi dhaifu ambao usingeweza kuhimili
vita kwa muda mrefu. Uchumi wao ulitegemea kilimo na biashara ndogo ndogo
zilizofanywa na wanajamii, ambao wakati wa vita walihitajika kuenda vitani badala
ya kuendeleza shughuli zao za kiuchumi. Hii ilimaanisha kuwa kipato chao kidogo
kingeweza kusaidia mapigano kwa muda mfupi tu. Wakati huo huo, Wajerumani
walikuwa na uchumi imara uliowawezesha kuhimili vita kwa muda mrefu, kwani
nchi ya Ujerumani ilikuwa na uwezo wa kuwasaidia kifedha.
53
03/10/2024 18:15:14
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 53 03/10/2024 18:15:14
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 53

