Page 66 - Historia_Maadili
P. 66
Watanzania walilazimishwa kujenga miundombinu mbalimbali. Kwa mfano, watu
walijenga reli ya kati na Tanga, 1893-1911, kwa lazima na kuchapwa viboko pale
walipogoma kufanya kazi. Watu walilazimika kufanya kazi hata pale walipokuwa
wamechoka. Hali hii iliwakasirisha sana Watanzania.
Kudhihakiwa kwa mila na desturi za Watanzania: Wakoloni kupitia Wamisionari
FOR ONLINE READING ONLY
walipiga marufuku mila na desturi za Kiafrika. Kwa mfano, majina ya Kiafrika
yalionekana ni ya “kishenzi” na vilevile dini za jadi zilionekana ni za “kishenzi”.
Baadhi ya vyakula, nguo, lugha na sanaa vilipigwa marufuku. Badala yake walitilia
mkazo matumizi ya utamaduni wa kigeni. Dini za Ukristo na Uislamu zikawa ni
alama ya ustaarabu kwa Waafrika waliozifuata imani hizi. Hali hii iliwakasirisha
wanajamii na hivyo hawakuwa tayari kuona mila na desturi zao zikidharaulika. Kwa
mfano, moja ya sababu za kuibuka kwa vita vya Maji Maji katika eneo la Songea
ni kudhihakiwa na kuchomwa moto kwa eneo la ibada za jadi za jamii ya Wangoni
huko Maposeni karibu na Peramiho. Kitendo hicho kilisababisha kuuawa kwa padri
mwenye asili ya Ujerumani aliyeitwa Franciscus Leuthner pamoja na kuvunjwa kwa
kanisa katika eneo la Peramiho tarehe 10 Septemba mwaka 1905.
Kuongozwa na wakoloni: Wakoloni walitaka kutawala Tanganyika na Zanzibar
kwa muda mrefu. Hivyo, mifumo ya kiutawala haikutoa nafasi kwa Waafrika
kuendelea na utamaduni wao wa kuongozwa na viongozi wao wa jadi. Utawala wa
kikoloni ulidhihirisha kupotea kwa uhuru wa Watanzania kwani hawakuwa huru.
Hata pale viongozi wao wa jadi walipokuwa wakitawala kupitia mfumo wa uwakala.
Hata hivyo, uamuzi wote ulitolewa na wakoloni kupitia gavana au wasaidizi wake
kama wakuu wa mikoa (provincial commissioners) au wakuu wa wilaya (district
commissioners). Mambo haya yaliwaudhi sana wananchi na kuamua kutafuta
uhuru wao uliopotea. Mbaya zaidi hata pale wakoloni walipotakiwa kuwaandaa
Watanganyika na Wazanzibari kujitawala, wao waliendelea kuwatawala kwa manufaa
yao. Kwa mfano, Umoja wa Mataifa uliwapa Waingereza jukumu la kuisimamia na
kuiandaa Tanganyika kujitawala baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, badala
yake hawakuwa na mpango wa kuondoka na kutoa uhuru kwa Watanganyika. Hivyo,
waliendelea kujiimarisha kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni ili kuendelea kuitawala
Tanganyika kwa manufaa ya taifa lao la Uingereza. Hivyo, hali hii iliwakasirisha
Watanganyika na kuamua kuanzisha harakati za kudai uhuru.
Kazi ya kufanya 4.1
Soma matini kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo mitandao ili kubainisha misingi
mingine ya kudai uhuru wa Tanganyika na Zanzibar.
58
03/10/2024 18:15:14
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 58 03/10/2024 18:15:14
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 58

