Page 62 - Historia_Maadili
P. 62
Kazi ya kufanya 3.6
Fanya utafiti kupitia vyanzo mbalimbali vya taarifa ili kubaini sababu nyingine
zilizosababisha Watanzania kushindwa katika vita dhidi ya uvamizi wa kikoloni.
FOR ONLINE READING ONLY
Zoezi la 3.4
1. Linganisha vita ya Maji Maji na vita vya jamii nyingine za Kitanzania
zilizopinga uvamizi wa Wajerumani.
2. Fafanua maadili ambayo viongozi wa sasa wanaweza kujifunza kutoka kwa
viongozi wa jamii za Kitanzania waliopinga uvamizi wa kikoloni.
3. Eleza athari za uvamizi wa kikoloni katika jamii za Kitanzania.
Matokeo ya kupinga uvamizi wa kikoloni
Ni muhimu kukumbuka kuwa jamii za Kitanzania zilipambana vikali kuupinga ukoloni.
Kutokana na matumizi ya silaha duni za jadi, wakoloni walifanikiwa kuzishinda na
kuendelea kuzitawala. Katika kipindi chote cha vita, wananchi walijitoa kwa hali na
mali, wakiongozwa na viongozi wa jadi waliotetea uhuru, haki, masilahi na utu wao.
Matokeo ya mapambano hayo yalikuwa kama ifuatavyo:
Shughuli za uzalishaji mali zilisimama: Kipindi chote cha vita, badala ya kuzalisha,
muda mwingi ulitumika katika kujipanga kivita na kupigana. Hali hii ilisababisha
upungufu wa chakula na kuleta njaa kubwa, kama ilivyotokea wakati wa Vita vya
Maji Maji, ambapo njaa hiyo iliitwa “Fungafunga.” Njaa hii iliwafanya watu kuishiwa
nguvu na kufa; wengine walilazimika kula wadudu, mizizi ya miti na matunda ya
msituni, ambayo mengine yalikuwa na sumu.
Kutumikishwa kwa nguvu kazi ya vijana: Wanaume, hasa vijana wenye nguvu,
walisafirishwa mbali na makazi yao na kutumikishwa katika mashamba ya walowezi.
Pia, kulizuka maradhi ya mlipuko kama vile mafua makali, kichocho na kuhara.
Maradhi haya yalisambaa kwa haraka kwa sababu wananchi wengi walikimbia makazi
yao na kushindwa kupata maji salama na chakula.
Vifo kutokana na wanyama pori: Athari nyingine ya vita ilikuwa vifo
vilivyosababishwa na wanyama pori. Wakati wa vita, wapiganaji walitumia muda
mwingi msituni. Wanawake na watoto pia walikimbilia maeneo ya msituni na
mapangoni kujificha na wengi wao walijeruhiwa au kuuawa na wanyama wakali
wa msituni.
54
03/10/2024 18:15:14
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 54
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 54 03/10/2024 18:15:14

