Page 65 - Historia_Maadili
P. 65
chini ya Sultani Jamshid bin Abdullah Al Said tarehe 10 Desemba, 1963. Waziri Mkuu
wa Serikali ya Sultani aliitwa Mohamed Shamte kutoka ZPPP. Hata hivyo, harakati
za ukombozi wa Waafrika walio wengi zilifanikiwa kupitia Mapinduzi Matukufu
ya tarehe 12 Januari, 1964. Hivyo, ilikuwa ni jukumu muhimu kwa wananchi wa
Tanganyika na Zanzibar kuanzisha harakati za kuudai uhuru na kujikomboa kutoka
katika ukoloni wa Kisultani na Kiingereza.
FOR ONLINE READING ONLY
Misingi ya kudai uhuru wa Tanganyika na Zanzibar
Harakati za kudai uhuru wa Tanganyika na Zanzibar zilianza mara tu baada ya
kuanzishwa kwa serikali za kikoloni. Watanzania wengi hawakupendezwa na tawala
za kikoloni na hivyo wakaanzisha mapambano na harakati za kupinga tawala hizo.
Zipo sababu kadhaa zilizowafanya Watanzania kuanzisha harakati za kudai uhuru
wao. Hii ni pamoja na kuupinga unyonyaji wa mali na rasilimali za wananchi, sera
za kibaguzi na za kinyonyaji za wakoloni, ukandamizaji wa Waafrika, kuzilinda mila
na desturi dhidi ya tamaduni za kigeni na kutaka kuishi kwa amani katika taifa huru
linaloongozwa na viongozi wa Kitanzania. Sababu hizi zinafafanuliwa zaidi katika
sehemu zifuatazo:
Unyonyaji wa mali na rasilimali: Mfumo wa kikoloni ulikuwa wa kinyanyasaji
na kinyonyaji. Watanzania walinyonywa katika nchi yao. Mathalani, walifanya kazi
maeneo mbalimbali kama vile mashambani, migodini na sehemu nyingine za nchi bila
kupata ujira unaostahili. Pia, mfumo wa kikoloni uliwalazimisha wananchi kulima
mazao yaliyoletwa na wakoloni kwa ajili ya viwanda vyao vilivyopo Ulaya. Sera za
kikoloni zilizokuwa za kinyonyaji zilisababisha Watanzania kuachana na malengo ya
kufanya kazi kwa ajili ya kuzalisha mazao yaliyoletwa na wakoloni. Hali hii ilijenga
msingi mmojawapo katika harakati za kudai uhuru wa Tanganyika na Zanzibar.
Sera za kibaguzi: Katika kipindi cha ukoloni, sera mbalimbali za kibaguzi zilianzishwa
kupitia huduma za jamii na ajira. Kwa mfano, wananchi walibaguliwa katika kupata
huduma za kijamii kama vile; afya, elimu na makazi. Wazungu, Waarabu na Waasia
walipewa huduma bora wakati Waafrika wakipewa huduma duni au kutokupewa
kabisa. Vilevile, kulikuwa na ubaguzi katika kupata ajira zenye hadhi. Kwa ujumla,
Waafrika walipewa kazi za usaidizi na zile za ngazi ya chini sana zilizosababisha
kulipwa ujira mdogo usioendana na uzito wa kazi walizokuwa wakifanya. Hali hii
ilisababisha baadhi ya wananchi kususia bidhaa za kikoloni kama njia ya kupinga
sera za kibaguzi za wakoloni.
Ukandamizwaji wa Waafrika: Wakoloni walipofika walianza kupora ardhi nzuri
ya uzalishaji mali kutoka kwa wenyeji. Hivyo, ili watu waweze kuishi, iliwalazimu
kufanya kazi katika mashamba ya wakoloni kwa ujira mdogo na wakati mwingine bila
malipo. Pia, serikali za kikoloni ziliwatoza kodi wananchi kwa nguvu na kuwafanyisha
kazi katika mashamba yao kwa ujira mdogo. Vilevile, katika maeneo mengine,
57
03/10/2024 18:15:14
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 57 03/10/2024 18:15:14
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 57

