Page 63 - Historia_Maadili
P. 63
Hofu miongoni mwa Watanzania: Vita vilisababisha kujengeka kwa hofu miongoni
mwa Watanzania. Kutokana na kushindwa kwa mapambano, watu wengi walipata
hofu ya kupigana tena na Wazungu.
Mateso na vifo vingi: Vita vya kupinga uvamizi wa wakoloni vilisababisha maelfu ya
vifo katika mapambano, kukamatwa kwa mateka, kunyongwa na vifo vilivyotokana
na njaa wakati na baada ya vita. Vilevile, vita viliathiri uzalishaji wa mazao ya
FOR ONLINE READING ONLY
biashara kama vile pamba, mkonge na mpira na pia iligharimu serikali ya kikoloni
kiasi kikubwa cha fedha kugharamia vita. Kwa sababu hiyo, Wajerumani walilazimika
kufanya mabadiliko katika sera zao za utawala na uchumi ili kupunguza migogoro
na wananchi.
Mwamko mpya wa harakati za uhuru: Ingawa jamii za Kitanzania zilishindwa
katika mapambano ya awali dhidi ya uvamizi wa kikoloni, mapambano hayo yaliacha
alama muhimu katika historia. Jamii hizi zilionesha ujasiri na dhamira ya kweli ya
kupinga ukandamizaji wa kigeni. Hali hii ilichochea mwamko mpya wa wapigania
uhuru wa baadaye, ambao walijifunza mengi kutoka kwa harakati hizo za kitaifa za
kudai uhuru.
Kumbukumbu muhimu katika historia ya Tanzania: Hapana shaka kwamba vita
vya kupinga ukoloni ni kumbukumbu muhimu katika historia ya Tanzania inayostahili
kuheshimiwa na yeyote anayethamini utu, uhuru, haki, heshima na usawa. Vita
hivyo ni kielelezo halisi cha Watanzania kukataa utawala wa kikoloni. Wajerumani
walijifunza kwamba mababu na mabibi zetu walikuwa tayari kuutetea na kuulinda
uhuru na rasilimali zao. Miaka mingi imepita tangu vita hivyo kutokea na kila
Mtanzania anapaswa kujiuliza ni mafundisho yapi anaweza kujifunza kutokana na
matukio hayo. Je, bado tunao ule moyo wa ushujaa, uzalendo, heshima na usawa
kama ilivyokuwa enzi za mababu na mabibi zetu?
Zoezi la marudio
1. Tofautisha kati ya maadili ya kikoloni na maadili ya jamii za Kitanzania
wakati ukoloni unaingia.
2. Eleza sababu za kushindwa kwa mapambano ya awali ya jamii za Kitanzania
dhidi ya uvamivi wa kikoloni.
3. Eleza jinsi viongozi wa sasa wanapaswa kutetea masilahi ya wananchi kwa
ujasiri na uzalendo.
4. Bainisha vitendo vya kijasiri vilivyooneshwa na viongozi wa jamii za
Kitanzania waliongoza mapambano ya awali dhidi ya uvamizi wa kikoloni.
5. Je, unafikiri ni namna gani mbinu ya jadi ya kivita iliyotumiwa na
Kinjeketile ilisaidia katika kupinga uvamizi wa Wajerumani?
6. Ni funzo gani viongozi wa sasa wanaweza kujifunza kutoka kwa jamii za
Kitanzania zilizopinga uvamizi wa Wajerumani?
55
03/10/2024 18:15:14
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 55 03/10/2024 18:15:14
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 55

