Page 72 - Historia_Maadili
P. 72

Kwa upande wa Tanganyika, mnamo mwaka 1935 ilianzishwa Klabu ya Waafrika
          yenye jina la Young African Sports Club ambayo pamoja na kushiriki mashindano ya
          mpira wa miguu ilikuwa na lengo la kuwaunganisha Waafrika kujadili masilahi yao,
          matatizo yao na kuimarisha ushirikiano katika utatuzi wa changamoto mbalimbali.
          Aidha, vilabu hivi vilichangia kwa kiasi kikubwa kuhamasisha wananchi kujiunga
        FOR ONLINE READING ONLY
          na Jumuiya za Waafrika kama vile; African Association, Shirazi Association na
          TAA na baada ya jumuiya hizo kuwa vyama vya kupigania uhuru.  Pia, vilabu hivi
          vilitoa mchango mkubwa wa kuchangisha fedha kwa wanachama wao pamoja na
          kuwahamasisha kujiunga na vyama vya TANU na ASP.



           Kazi ya kufanya 4.3


            Soma matini kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo mitandao, kisha fafanua jinsi
            vikundi na vyama vya kidini vilivyochangia katika harakati za kudai uhuru wa
            Tanganyika na Zanzibar.



          Vyombo vya habari

          Kuanzishwa kwa vyombo vya habari katika Tanganyika na Zanzibar kuliongeza na
          kuimarisha harakati za Waafrika katika kupigania uhuru wao. Kabla ya kuanzishwa
          kwa vyombo hivi vya Waafrika, kulikuwepo vyombo vya habari vilivyokuwa
          vimeanzishwa na serikali ya kikoloni. Hata hivyo, vyombo hivyo vya kikoloni
          havikutoa habari kuhusu harakati za kudai uhuru wa Tanganyika na Zanzibar, bali
          vilijikita zaidi katika kuwasifia wakoloni na kuelezea matukio ya huko Ulaya.


          Kutokana na changamoto hii, Waafrika wakaona kuwa kuna umuhimu wa kuunda
          na kuanzisha vyombo vya habari vyao wenyewe. Mfano wa vyombo hivyo ni gazeti
          la Kwetu, lililoanzishwa na jumuiya ya African Association (AA) mwaka 1937 na
          Sauti ya TANU, ambalo lilihaririwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka
          1957. Kazi hii ya uhariri ilimletea matatizo Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
          baada ya kuchapisha taarifa ambayo haikuupendeza utawala wa Waingereza. Hivyo,
          mnamo tarehe 9 Julai 1958, Julius Kambarage Nyerere alishtakiwa katika Mahakama
          ya Dar es Salaam kwa makosa ya uchochezi dhidi ya serikali ya kikoloni. Tarehe 12
          Agosti 1958, Mwalimu Nyerere alihukumiwa kulipa faini ya shilingi elfu tatu, sawa

          na paundi 150 za Uingereza, au kwenda jela miezi sita kama angeshindwa kulipa.
          Wanachama na wapenzi wa TANU walichanga fedha na kumsaidia kulipa faini hiyo
          ili kumnusuru Mwalimu Nyerere asitumikie kifungo cha jela.



                                                  64




                                                                                        03/10/2024   18:15:15
   HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd   64
   HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd   64                                         03/10/2024   18:15:15
   67   68   69   70   71   72   73   74   75   76   77