Page 78 - Historia_Maadili
P. 78
maadili ya umoja yaliyodumu kwa muda mrefu. Maadili haya ya umoja yalikuwa
muhimu katika kujenga mshikamano miongoni mwa jamii za Kitanzania. Pia, ilisaidia
kudumisha nguvu ya kitaifa, kupinga ukoloni na kudai uhuru wa Tanganyika na
Zanzibar. Kwa hivyo, harakati za kupinga uvamizi na utawala wa kikoloni na juhudi
za kudai uhuru, zilichangia katika kudumisha maadili ya umoja na nguvu ya kitaifa
katika kudai uhuru wa nchi zao.
FOR ONLINE READING ONLY
Utu
Uvamizi na utawala wa kikoloni ulikuwa ni wa kimabavu na uliweka mifumo ya
kuwanyanyasa, kuwanyonya na kuwakandamiza Watanzania. Hali hii ilitweza utu
wao. Pia, Watanzania walidhalilishwa kwa adhabu kali za viboko hadharani pale
waliposhindwa kulipa kodi au kufanya makosa mengine. Adhabu hizi zilitolewa kwa
kuwavua nguo na kuwachapa mijeledi hadharani, kitendo kilichowachukiza sana
wananchi kwa kuwa kilitweza na kudhalilisha utu wao.
Kwa sababu hii, wananchi walipinga na kupambana ili kuonesha hisia zao za
kuchoshwa na dhuluma na manyanyaso ya wakoloni. Harakati mbalimbali dhidi ya
uvamizi na matendo maovu ya wakoloni zilitokea karibu kila sehemu ya Tanganyika.
Ukoloni na mifumo yake iliathiri sana utu wa Waafrika na hivyo kuamsha ari ya
kupata uhuru ili kutunza maadili ya utu yaliyokuwa yamejengwa na jamii za asili
za Tanganyika na Zanzibar. Kwa hivyo, harakati za kupinga ukoloni pia zilichangia
katika utunzaji na udumishaji wa maadili ya utu, kwani Watanzania hawakuwa tayari
kuona utu wao au maadili yao yakipotea.
Mshikamano
Harakati za kupinga ukoloni na kupigania uhuru wa Tanganyika na Zanzibar
zilichangia pia katika kutunza maadili ya mshikamano miongoni mwa jamii za
Kitanzania. Wakati wa kupinga uvamizi, viongozi waliwaunganisha watu katika
jamii zao ili kuwa na nguvu za kupambana na uvamizi wa wakoloni. Viongozi wa
jamii kama vile Mtwa Mkwawa wa kabila la Wahehe, Mangi Meli wa Old Moshi,
Mtemi Isike wa Unyanyembe na viongozi wengine walihamasisha watu wao
kushikamana ili kukabiliana na uvamizi wa wakoloni wa Kijerumani. Viongozi
hawa walitambua kwamba adui yao alikuwa na nguvu za kijeshi. Hivyo, jamii zao
zilihitaji mshikamano ili kuweza kupambana na wakoloni hao. Kuyatunza maadili ya
mshikamano kuliwawezesha kutoa upinzani mkali kwa wavamizi, ingawa baadaye
hawakufanikiwa kutokana na sababu mbalimbali.
Aidha, wakati wa harakati za kudai uhuru wa Tanganyika na Zanzibar, viongozi
walihimiza mshikamano wa Watanzania wote ili kuwezesha Tanganyika na Zanzibar
kupata uhuru. Katika kuimarisha mshikamano dhidi ya utawala wa Waingereza,
wananchi walijiunga katika makundi mbalimbali ya kimasilahi, ambapo wakulima
wa mazao makuu ya biashara waliunda vyama vya ushirika kupigania bei nzuri ya
70
03/10/2024 18:15:16
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 70 03/10/2024 18:15:16
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 70

