Page 79 - Historia_Maadili
P. 79
mazao na unafuu wa pembejeo za kilimo. Vyama mashuhuri vilikuwa ni pamoja na
Kilimanjaro Native Cooperative Union (KNCU), Victoria Federation of Cooperative
Union (VFCU), Bukoba Bahaya Union na Umoja wa Meru. Vyama hivi na vingine
vilijenga mshikamano miongoni mwa wananchi na wakati wa harakati za kupigania
uhuru, vilitoa mchango mkubwa wa kisiasa na hatimaye kuwa sehemu ya chama
cha ukombozi cha Tanganyika African National Union (TANU). Hivyo, harakati
FOR ONLINE READING ONLY
za kupinga uvamizi wa wakoloni na kupigania uhuru zilichangia katika utunzaji wa
maadili ya mshikamano ambayo yanaenziwa na taifa letu hadi sasa.
Kiswahili
Harakati za kupinga ukoloni na kupigania uhuru wa Tanganyika na Zanzibar zilitumia
lugha ya Kiswahili kwa namna mbalimbali. Mathalani, Kiswahili kilitumika kusaidia
kuleta umoja na mshikamano miongoni mwa wanachama wa TANU na ASP pamoja
na wananchi wote. Lugha ya Kiswahili pia ilitumika kuwaunganisha wananchi wa
Tanganyika na Zanzibar ili kupigania uhuru wa nchi zao. Wananchi wa nchi hizo,
licha ya kwamba walitoka katika makabila na jamii tofauti, lugha ya Kiswahili
iliwaunganisha na kuwafanya kuwa kitu kimoja katika kupigania nchi zao. Aidha,
lugha ya Kiswahili ilisaidia kupeleka ujumbe kwa Watanganyika na Wazanzibari
kwani ilitumika na wengi. Mbinu na mikakati iliyotolewa kuhusu uzalendo na ari
ya kujitolea kupambana na ukoloni iliwasilishwa kwa kutumia lugha ya Kiswahili.
Vilevile, katika harakati za kupambana na ukoloni, nyimbo, hasa taarabu, zilitumia
lugha ya Kiswahili kupeleka ujumbe. Vyombo vya habari, kama vile magazeti ya
Afrika Kwetu, Mkombozi, Mwiba, Sauti ya Afro-Shirazi, Ukombozi na Sauti ya
Jogoo, vilitumia Kiswahili kuelimisha na kutoa habari kwa wananchi kuhusu harakati
za kupigania uhuru.
Aidha, sera na itikadi za TANU na ASP zilielezwa kwa lugha rahisi ya Kiswahili,
hivyo kurahisisha ufikishaji wa ujumbe kwa wananchi. Viongozi waliamua kutumia
lugha ya Kiswahili ili kueneza na kufikisha kwa urahisi sera za vyama vyao kwa
wananchi. Wananchi walihamasishwa kutumia Kiswahili katika mawasiliano, jambo
lililosaidia kuondoa hali ya ukabila na ubaguzi wakati wa kupigania uhuru. Kiswahili
kilikuwa nguzo muhimu katika kufikisha taarifa na habari juu ya harakati za kupigania
uhuru na kilisaidia kuwaunganisha wananchi hadi kufikia hatua ya kupatikana kwa
uhuru wa Tanganyika na Zanzibar.
Kujenga uzalendo
Harakati za kupinga ukoloni zilihusisha kupinga sera na hata kuhusisha kupigana
vita dhidi ya wakoloni. Katika harakati za kupinga ukoloni, Watanzania walionesha
na kujenga uzalendo kwa jamii zao pale waliposimama kidete kuupinga uvamizi na
utawala wa kikoloni kwa sera zao za unyonyaji na ukandamizaji. Pia, Watanzania
walipinga kuingia kwa utawala wa kikoloni kwa kupambana kivita dhidi ya wavamizi
71
03/10/2024 18:15:16
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 71 03/10/2024 18:15:16
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 71

