Page 84 - Historia_Maadili
P. 84
kisiasa, kijamii, kiutamaduni na kiuchumi kwa Taifa huru la Tanzania. Mifumo hiyo
ilijengwa chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa upande wa
Tanganyika na Sheikh Abeid Amani Karume kwa upande wa Zanzibar. Katika kipindi
hiki, vyama vya TANU na ASP vililenga kujenga taifa lenye kuzingatia maadili ya
usawa, utu, heshima kwa kila mtu, haki na wajibu. Aidha, umoja, uzalendo, kujitolea
na kupenda kazi vilikuwa miongoni mwa maadili yaliyojengwa, yakiongozwa na kauli
FOR ONLINE READING ONLY
mbiu iliyotangaza vita dhidi ya maadui watatu: umaskini, ujinga na maradhi. Kila
mwananchi alisisitizwa kuzingatia maadili ya Kitanzania na kujiepusha na unyonyaji,
rushwa, ukabila na uzembe. Mifumo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii iliyojengwa
katika kipindi hiki imefafanuliwa vema katika sehemu zinazofuata.
Kazi ya kufanya 5.1
Pitia mtandao au vifaa vingine vya TEHAMA, sikiliza hotuba za waasisi wa taifa
ambao ni Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume
kuhusu umuhimu wa maadili katika ujenzi wa taifa huru. Baada ya kusikiliza
hotuba fanya yafuatayo:
(a) Bainisha mambo yaliyokugusa katika hotuba hizo.
(b) Kama ungekuwepo kipindi hicho ungependa kuwauliza mambo gani
waasisi wa taifa letu?
(c) Eleza namna maadili yaliyozungumzwa katika hotuba hizo bado ni
muhimu katika Tanzania ya sasa.
Kisiasa
Tanganyika kuwa Jamhuri: Tanganyika ilikuwa Jamhuri mwaka 1962. Jamhuri
ni serikali ya watu yenye mamlaka kamili, inayoongozwa na Rais. Msukumo wa
Tanganyika kuwa Jamhuri ulitokana na sababu mbalimbali. Kwanza, ilihitajika kuwa
na uhuru kamili wa serikali, badala ya kuwa na uhuru wa bendera chini ya uongozi
wa Malkia wa Uingereza. Kabla ya Tanganyika kuwa Jamhuri, serikali ilikuwa
inaongozwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kama Waziri Mkuu, aliyekuwa
chini ya mamlaka ya Malkia wa Uingereza, huku Gavana wa kikoloni akiendelea kuwa
kiongozi mkuu wa nchi, akimwakilisha Malkia Elizabeth II wa Uingereza. Gavana
huyo aliendelea kutekeleza baadhi ya majukumu ya kiserikali, hivyo kumfanya Waziri
Mkuu kukosa mamlaka kamili.
Pia, Tanganyika ilitaka kutambulika katika jumuiya za kimataifa kama nchi yenye
uhuru kamili na kuwa Jamhuri ilikuwa njia ya kufanikisha hilo, kwani iliwapa fursa ya
kushiriki katika mikutano na jumuiya hizo za kimataifa. Vilevile, wananchi walitaka
76
03/10/2024 18:15:17
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 76
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 76 03/10/2024 18:15:17

