Page 88 - Historia_Maadili
P. 88
mfumo mpya wa uchumi. Mifumo ya uchumi iliyobuniwa katika kipindi hiki ililenga
kujenga jamii ya watu wanaojitegemea. Kwa mfano, Tanganyika ilianzisha Mpango
wa Maendeleo wa Miaka Mitatu uliotekelezwa kuanzia mwaka 1961 hadi 1964.
Baada ya mpango huo, ulianzishwa Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka
Mitano (1964–1969), ambao ulitakiwa kufuatiwa na Mpango wa Pili wa Miaka
Mitano. Mipango hii ililenga, miongoni mwa mambo mengine, kuleta maendeleo
FOR ONLINE READING ONLY
ya kiuchumi ya taifa huru.
Kuanzia mwaka 1963 hadi 1965, sera ya maendeleo vijijini ilianzishwa. Hii ilikuwa
ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitatu. Sera hii
ililenga kuwaweka wananchi katika vijiji ili kuimarisha kilimo kwa kutumia teknolojia
ya kisasa. Serikali iliamini kuwa kuwakusanya wananchi vijijini kungewezesha
kurahisisha utoaji wa huduma za ugani, elimu na miundombinu muhimu. Hii ilisaidia
pia kuhamasisha maendeleo ya kilimo na kuwapa wananchi fursa ya kushiriki
kikamilifu katika ujenzi wa taifa. Kilimo kilipewa kipaumbele na kuhimizwa kuwa
uti wa mgongo wa taifa, huku wakulima wakihamasishwa kulima mazao ya biashara
na chakula. Kupitia uhamasishaji huu, walipatiwa pembejeo na kupewa uhakika wa
masoko ya mazao yao kupitia vyama vya ushirika.
Vilevile, viwanda mbalimbali vilijengwa Tanganyika. Kwa mfano, Kiwanda cha
Nguo cha Urafiki kilijengwa mwaka 1966 chini ya makubaliano ya urafiki kati ya
Tanzania na China. Hiki kilikuwa kiwanda kamilifu chenye mitambo ya kisasa ya
utengenezaji wa nguo. Viwanda vingine vingi katika kipindi hiki vilimilikiwa na
wageni na vilijikita katika uzalishaji wa bidhaa kama vile vinywaji, uchakataji wa
malighafi za kilimo na bidhaa za matumizi kama Coca-Cola, East African Breweries,
Tanganyika Packers, British American Tobacco, Metal Box na Bata Shoes, Ubungo
Fram Impelements na National Printing Company.
Aidha, serikali ilijikita katika kuhakikisha taasisi za fedha zinaendelezwa ili kuwa
mihimili muhimu katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya taifa. Serikali ilianzisha
Benki Kuu ya Tanzania mwaka 1966 ili kusimamia masuala muhimu ya kifedha
nchini. Pia sekta nyingine, kama vile uvuvi, nishati na madini, zilipewa kipaumbele.
Kazi ya kufanya 5.3
Tembelea wazee na watu wengine wenye ufahamu kuhusu mifumo ya uchumi
iliyojengwa mara baada ya uhuru, kisha fanya mahojiano nao kuhusu mifumo
hiyo kwa kuzingatia mambo yafuatayo:
(a) Maisha ya jamii kiuchumi mara baada ya uhuru;
(b) Mifumo ya kiuchumi iliyojengwa na jinsi ilivyoinufaisha jamii; na
(c) Andika ripoti ya uchunguzi wako.
80
03/10/2024 18:15:18
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 80 03/10/2024 18:15:18
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 80

