Page 93 - Historia_Maadili
P. 93
za kupata huduma bora, hasa katika utoaji wa mikopo. Aidha, baadhi ya watu ndani
ya chama walionesha nia ya kupata uongozi ili kujinufaisha binafsi na kujilimbikizia
mali. Baadhi ya mambo yaliyojitokeza baada ya uhuru ni kama yafuatayo:
(a) Kujengeka kwa matabaka ya kiuchumi, kisiasa na kijamii, kinyume na
mfumo wa kijamii uliokuwepo kabla ya uhuru ambapo jamii iliishi kwa
FOR ONLINE READING ONLY
umoja, udugu, upendo na kushirikiana; na
(b) Baadhi ya viongozi na watumishi wa umma walianza kukiuka maadili ya
utumishi wa umma na kutumia nafasi walizopewa kama vitega uchumi ili
kujinufaisha wenyewe.
Kutokana na kuongezeka kwa matabaka, ubadhirifu wa mali na baadhi ya viongozi
wa umma kuanza kujilimbikizia mali, Serikali ya Awamu ya Kwanza ilichukua hatua
ya kuunda tume. Mwaka 1966, Mwalimu Julius K. Nyerere aliunda Tume ya Rais
ya Kudumu ya Uchunguzi (The Presidential Permanent Commission of Enquiry) ili
kuchunguza mwenendo wa viongozi na watumishi wa umma waliokuwa wakikiuka
maadili, kujilimbikizia mali na kutumia madaraka vibaya kinyume na miiko ya chama
cha TANU, ambacho mara kwa mara kilikemea vitendo vya rushwa. Tume ya Rais ya
Kudumu ya Uchunguzi ya mwaka 1966 ilichangia Kamati Kuu ya TANU kutangaza
Azimio la Arusha mwaka 1967, lililoweka miiko mbalimbali yenye misingi ya utu na
usawa katika jamii, mambo ambayo yalisaidia katika mapambano dhidi ya rushwa.
Kwa upande wa Zanzibar, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliweka sera ya umiliki
wa ardhi chini ya tangazo la tarehe 8 Machi 1964. Kupitia tangazo hilo, Serikali ya
Sheikh Abeid Amani Karume ilitaifisha mali zisizohamishika kama ardhi, mashamba
na majengo na kuweka mpango wa ugawaji ardhi kwa utaratibu wa hekari tatu kwa
kila familia. Sheria hiyo ilitoa fursa kwa ardhi iliyotaifishwa kugawanywa kwa
familia na watu masikini wasio na ardhi. Kabla ya mapinduzi, asilimia kubwa ya
ardhi, yakiwemo mashamba ya mikarafuu na minazi, ilikuwa ikimilikiwa na watu
wachache hasa Waarabu.
Ugawaji wa ardhi ulifanyika kupitia amri ya utaifishaji wa mali zisizohamishika, “The
Confiscation of Immovable Property Decree 1964,” na amri ya ugawaji wa ardhi, “The
Land Distribution Decree 1966.” Ugawaji huo ulianza huko Dole tarehe 11 Novemba
1965, ambapo wananchi waligawiwa hekari tatu kila familia. Hadi kufikia mwaka
1973, zaidi ya hekari 24,000 zilikuwa zimetolewa kwa Wazanzibari.
85
03/10/2024 18:15:18
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 85
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 85 03/10/2024 18:15:18

