Page 92 - Historia_Maadili
P. 92
Mikakati ya ujenzi wa taifa
Kati ya mwaka 1961 hadi 1966, serikali ya Tanzania iliweka mikakati mbalimbali ya
kujenga taifa linalojitegemea. Mojawapo ya mikakati hiyo ilikuwa kuanzisha mfumo
wa chama kimoja cha siasa, Chama cha TANU, ambacho kilikuwa chama pekee
kilichoruhusiwa kufanya shughuli za kisiasa Tanganyika (Tanzania Bara) na Chama
cha ASP kwa upande wa Zanzibar. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
FOR ONLINE READING ONLY
iliona mfumo wa chama kimoja kama njia bora ya kuleta mshikamano na umoja wa
kitaifa. Mfumo huu ulilenga kuondoa siasa za kibaguzi na kuipunguza migogoro ya
kisiasa ambayo ingeweza kutishia umoja wa taifa changa. Aidha, mfumo wa chama
kimoja ulikuwa njia ya kuhamasisha jamii kushiriki katika shughuli za maendeleo.
Vyama vya TANU na ASP vilikemea ukiukwaji wa maadili na muundo wa kijamii,
kisiasa na kiuchumi ulioathiriwa kutoka mfumo wa kikoloni. Mfumo wa kikoloni
ulikuwa na ubaguzi na vitendo vya rushwa. Kutokana na hali hii, TANU ilitengeneza
kauli mbiu yake iliyosema, “Rushwa ni adui wa haki, sitatoa wala kupokea rushwa.”
Tanganyika iliendelea na mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa kwa kutumia Sheria
ya Kuzuia Rushwa (Sura ya 400) ya Mwaka 1958 (The Prevention of Corruption
Ordinance, PCO, of 1958), sheria iliyorithiwa kutoka kwa wakoloni.
Pia, mwaka 1962, serikali ilifuta mfumo wa uchifu katika uongozi wa nchi.
Kuondolewa kwa mfumo wa machifu, ambao ulikuwa sehemu muhimu ya utawala
wa kikoloni, kulikuwa na mkakati wa makusudi wa kulijenga taifa jipya. Machifu
walikuwa na nguvu kubwa katika jamii zao na mara nyingi walitumiwa na wakoloni
kama vibaraka wao. Lengo la kuondoa mfumo huu lilikuwa kuvunja mamlaka ya
kikabila na kuipa serikali kuu mamlaka ya kutawala maeneo yote, hivyo kuondoa
hisia za ukabila.
Vilevile, serikali ilianzisha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) tarehe 10 Julai, 1963. Jeshi
hili lilianzishwa kama sehemu ya mikakati ya kukuza uzalendo, maadili na ujenzi
wa taifa. Jeshi hili lililenga kutoa mafunzo ya kijeshi pamoja na stadi za kazi kwa
vijana wa Kitanzania. Kupitia JKT, vijana walihamasishwa kushiriki katika ujenzi wa
miundombinu ya taifa, kama vile barabara, mashamba ya umma na miradi mingine
ya maendeleo. Jeshi hili lilitumika kama chombo cha kuimarisha nidhamu, uzalendo,
uvumilivu, kujitolea na uwajibikaji wa kijamii miongoni mwa vijana na kuwafanya
kuwa sehemu ya nguvu kazi na hazina ya taifa. Hivyo, JKT liliwajengea vijana
nidhamu, uzalendo, ukakamavu na kuwafundisha ujuzi hatimaye kuchangia katika
ulinzi wa Taifa na maendeleo ya kiuchumi.
Halikadhalika, miaka mitano baada ya uhuru wa Tanganyika, yaani mwaka 1966,
vitendo vya rushwa vilionekana kuongezeka na baadhi ya viongozi wa umma walianza
kujisahau. Tofauti kubwa kati ya watu wenye nacho na wasio nacho, pamoja na wenye
elimu na wasio na elimu, ilionekana kuongezeka. Watu waliosoma walikuwa na fursa
84
03/10/2024 18:15:18
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 84 03/10/2024 18:15:18
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 84

