Page 95 - Historia_Maadili
P. 95
Kuibuka kwa tabaka la mabepari uchwara: Kama ilivyokuwa katika nchi nyingine
nyingi za Afrika, tabaka jipya la mabepari uchwara waliokuwa wamechukua madaraka
serikalini walianza kutumia nyadhifa zao kujinufaisha. Wananchi walianza kushuhudia
viongozi wakiishi maisha ya anasa huku raia wa kawaida wakibaki masikini. Hali
hii ilikuwa tishio kwa umoja, maadili, amani na mshikamano uliokuwa unasisitizwa
na kujengwa mara baada ya uhuru.
FOR ONLINE READING ONLY
Hali mbaya ya uchumi: Katika kipindi hiki, hali mbaya ya uchumi ilitokea na kuathiri
sana upatikanaji wa huduma za kijamii kama elimu, afya na nyinginezo zinazotolewa
na serikali. Tatizo hili lilisababisha pia ukosefu wa wataalamu, teknolojia duni,
kuongezeka kwa maradhi, ujinga na umaskini, pamoja na kuwapo kwa miundombinu
mibovu. Uchumi ulitegemea kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa malighafi badala ya
bidhaa za viwandani. Hata hivyo, serikali ilianza kuchukua hatua za mageuzi ili
kurekebisha changamoto hizi.
Serikali pia ilikabiliwa na changamoto za kifedha na kiutawala katika kutoa huduma
za afya kwa umma. Juhudi za kuanzisha zahanati na hospitali mpya zilikwamishwa na
upungufu wa vifaa na wahudumu wa afya wenye sifa. Hali hii ilisababisha huduma za
afya kutokidhi mahitaji katika baadhi ya maeneo. Pia, utegemezi wa misaada kutoka
mataifa mengine ulifanya utoaji wa huduma za afya na miradi mingine kudorora.
Uwapo wa vita baridi miongoni mwa mataifa makubwa duniani pia kuliathiri sera za
mambo ya nje za Tanzania. Hii ni kwa sababu nchi ilikuwa mwanachama wa Harakati
za Kutofungamana na Upande Wowote (Non-Alignment Movement, NAM). Hali hii
ilileta migogoro na mataifa makubwa yaliyokuwa yakihasimiana. Vilevile, utegemezi
wa misaada kutoka nje ulipunguza uhuru wa taifa wa kupanga na kuamua mambo
yake. Kwa mfano, mwaka 1965, Tanzania ilikumbwa na mgogoro wa kidiplomasia na
Uingereza, hali iliyosababisha Uingereza kusitisha misaada. Hii iliathiri utekelezaji
wa miradi mingi ya kimkakati nchini. Pamoja na changamoto hizi, mikakati ya awali
ya ujenzi wa taifa iliweka msingi muhimu kwa juhudi za baadaye za maendeleo.
Kazi ya kufanya 5.6
Tafuta taarifa kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo mtandao na bainisha
changamoto nyingine za ujenzi wa taifa na jinsi zilivyotatuliwa.
87
03/10/2024 18:15:19
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 87
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 87 03/10/2024 18:15:19

